Sunday, 16 November 2014

Hadithi ya kusisimua:MWANASHERIA KATILI


 Siku zilipita huku Mike akiwa bado likizo na alizidi kufurahia maisha yake ya pale nyumbani.Mara furaha ya Mike ikatoweka ghafla akawa ni mtu wa huzuni kila wakati.Kila muda Mike alit...okwa na machozi mfululizo akiwa chumbani kwake na kuendelea kumwomba Mungu.Jini Bahari alimtokea mara kwa mara na kumwambia kuwa….
“Usijali, haya ni matatizo tu yanayoletwa na wakubwa zangu.Si unakumbuka kabla sijakutorosha nilikwambia wakubwa watakufuata.Ila usife moyo ahadi yangu ipo pale pale,nitakusaidia mpaka mwisho.Chamsingi ufuate masharti yangu tu!kwanza hutakiwi kukata tamaa kwa jambo lolote,pili hutakiwi kutamani mali ya mtu na mwisho huruhusiwi kufanya mapenzi na mwanamke yeyote mpaka utakapomaliza chuo.
“Sawa Mke!we fuata tu ninayotaka na utafanikiwa maisha yako yote,usikate tamaa.”Furaha ya Mike ilipotea siku moja asubuhi akiwa nyumbani Uncle wake akijiandaa kwa safari.Mara akasikia kengele ikilia,alikimbia mbio kwenda kufungua mlango.
“Shikamooni!”Mike aliwasalimia watu waliosimama mbele ya mlango.
“Marahaba!baba yako yupo?”Walijibu vijana watatu hivi na mzee mmoja wa makamo kiasi.Walimuulizia Mr.Cheo,Mike aliogopa kidogo kwa kuwa wale watu walikuwa na bunduki pamoja na pingu mkononi.
“Yupo ndani”Mike alijibu huku akitetemeka.
“Nenda kamwite.”Mike alirudi ndani na kumwita Uncle wake.Uncle aliambatana na mkewe mpaka waliposimama wale watu.
“Sisi ni maafisa wa polisi na kuanzia sasa hivi upo chini ya ulinzi kwa kosa la kuingiza madawa ya kulevya nchini”
“Nani?mimi!!!”Uncle alishikwa na kigugumizi ghafla. “Mimi sifanyi biashara hizo.”
“Mume wangu hafanyi biashara hizo haramu yeye ana biashara zake halali kabisa,mnamwonea bure tu jamani!!”Mke wa Uncle aliwaambia wale polisi huku akilia kwa uchungu.
Wale polisi hawakutaka malumbano walimfunga Uncle pingu na kuondoka naye kwa kutumia gari ndogo waliokuja nao.
“Nyamaza kulia Aunt !!”Mike alimbembeleza Aunt yake aliyekuwa analia baada ya mumewe kuchukuliwa na polisi.Kesho yake asubuhi Aunt aliamka mapema na kujiandaa kwenda Kisutu maabusu kumsalimia mumewe na kujua mstakabali mzima wa kesi yake.
“We Mike utaenda Manzese kuwataarifu dada zako kuhusu matatizo yaliyomsibu Uncle wao.”Aunt alimtaarifu Mike kisha akaondoka.Mike naye akajiandaa na kwenda Manzese kuwataarifu dada zake.
Jioni walirejea pamoja mpaka nyumbani kwa Uncle wao.Mwezi mzima wa Decemba Uncle bado alikuwa maabusu na kesi ilisogezwa mbele kila wakati.Sikukuu za Chrismasi na mwaka mpya hazikuwa za furaha hata kidogo kutokana na matatizo yaliyompata Mr.Cheo.
Mke wa Uncle alitumia fedha nyingi kuendesha kesi ile kwa kuwahonga maaskari na majaji lakini bado Uncle hakuachiwa huru.Biashara zote za Uncle zilisimama kwa kutokuwa na msimamizi yeyote.Mwezi January ndio mwezi ambao Mike alitakiwa kurudi shuleni.
“Mike!hutoweza kwenda shule kwa sasa kwasababu ada hamna,pesa zote zimeishia kwenye kesi ya Uncle wako hivyo itakubidi usubiri kidogo.Biashara zote zimekwama wewe mwenyewe si unaona?”mke wa Uncle alimweleza Mike hayo kwa uchungu wa hali ya juu.Mike alisikitika mno baada ya kusikia kuwa hatokwenda shule kwa kipindi hicho.Dada yake aliyekuja toka Manzese alimbembeleza Mike na kumfaraji kila wakati.
Ilifikia hatua Mike akawa hali chakula pale nyumbani,yeye ni kulia tu! Kutokana na kesi ile familia ya akina Mike ilifilisika sana hadi kufikia hatua ya kuuza vitu vya ndani kama TV na deki,dishi na vitu vingine vya thamani ili kupata pesa za kumtoa Uncle ndani lakini ilishindikana.Siku moja Mike alipata taarifa toka kwa Aunt kuwa waalimu walimpigia simu na kumuulizia,yeye aliwaambia kuwa anaumwa.Mike alilia sana baada ya kusikia kuwa waalimu wamemuulizia lakini hakukua na njia yoyote ile ya kurudi shule kwasababu ada ilikuwa tatizo.
Mwezi wa tatu baada ya ushahidi kukamilika Uncle alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu.Familia ya Uncle ilisikitika sana ,kila wakati ikawa ni maombolezo pale nyumbani.Uncle alifungwa jela ya Keko kwa miezi mitatu na baadae akahamishiwa Segerea hapa hapa jijini Dar-es-salaam.Mwisho wa mwezi May mke wa Uncle alienda kumtembelea mumewe gerezani.Alipofika tu alipewa muda wa nusu saa kuzungumza naye.
“Mume wangu pole sana kwa maswahibu yaliyokukuta.Hebu nieleze ukweli wa jambo wa hili.Mimi ni mkeo halali wa ndoa na ninakupenda sana.Hivi ni kweli mume wangu ulikuwa unajihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya bila mimi kujua?”
“Nakuomba mke wangu unisikilizea tena kwa makini sana.Mimi si muuzaji wa madawa ya kulevya kama watu wanavyodhani.Nimewekewa kwenye mizigo yangu iliyotoka Nigeria.Na hii imesababishwa na mchungaji mmoja maarufu sana hapa Dar-es-salaam ambaye anatumia cheo cha uchungaji kama kivuli kumbe anafanya biashara haramu”
“Sasa mume wangu huyo mchungaji ni yupi na amekusababishia vipi mpaka leo upo hapa?”mke wa Uncle alimuuliza mumewe.
“Mke wangu huyo mchungaji nimeshakutana naye mara kadhaa nchini Nigeria.Na kwa kipindi chote hicho aliniambia kuwa anaenda nchini humo kwaajili ya ziara zake za kikazi.Mimi nilimwamini sana kwa kuwa ni mchungaji.
“Siku moja nikiwa nchini humo nilikutana na mchungaji huyo kwa mara nyingine tena.Lakini wakati huu aliniomba nimsaidie kuleta mzigo wake nchini na aliniahidi kunilipa pesa nyingi.Nilipotaka kujua ni mzigo gani naopaswa kuuchukua alikataa kuniambia kwa muda huo ila alinitaka tukutane siku inayofuata katika hoteli moja maarufu nchini humo.Kesho yake nilijiandaa kwenda kukutana na mchungaji huyo.
“Nilimpigia simu kumjulisha kuwa ndio nakuja.Aliniambia kuwa ameshafika ananisubiri.Nilipofika hotelini nilipokelewa na vijana wanne wenye miili ya miraba minne na kila mmoja alikuwa na bunduki yake kiunoni.Niliogopa kidogo,mara mmoja akaniuliza “We ndio Mr.Cheo?”
“Ndio!!”nilijibu huku nikitetemeka.
“Ok.karibu sana”
Niliwashangaa wale vijana kwa kuwa walizungumza Kiswahili fasaha. “Inaelekea hawa ni Watanzania”nilijisemea mwenyewe kimoyomoyo huku nikiwafuata nyuma.Tulipanda ngazi mpaka ghorofa ya juu na kuingia ndani.Nilimkuta mchungaji huyo akiwa anapunga upepo katika bustani ya mapumziko.Alinikaribisha kwa mbwembwe na furaha tele!
“Oooh!!!!karibu rafiki mpendwa!karibu sana”
“Asante sana”nilimjibu na kuketi juu ya sofa.Mara wakaja wasichana wawili na kuniuliza ninachohitaji kwa lugha ya kiingereza.Niliwajibu kuwa nahitaji juice baridi na mara moja wakaniletea.Yule mchungaji alivuta pumzi kidogo na kuniambia kuwa…..
“Utakapofanya kazi na mimi utakuwa bilionea siku chache zijazo”
“ We niambie ni mzigo gani naondoka nao maana kesho kutwa ndio narudi Dar!”nilimsihi yule mchungaji na badala ya kunijibu akaanza kecheka.
“Ha!ha!ha!ha!tulia kijana usiwe na papara,we malizia kinywaji chako nikakuoneshe mzigo wenyewe”
Niligugumia juice yote kisha tukainuka kuelekea nje ya hoteli.Tuliingia kwenye gari moja la kifahari na tukaanza safari ya kuelekea kaskazini mwa mji wa Abuja.Ndani ya dakika 20 tulikuwa barabarani,tulikata kushoto na kuicha barabara kuu tukaingia vichochori.Mara gari likafunga breki mbele ya bangaloo la nyumba ambayo kwa nje ilionekana ya zamani sana kama vile hawaishi watu.Tulipoingia tu ndani ile gari iliondoka zake,sikujua yule dereva wetu alielekea wapi?
Niliishangaa sana ile nyumba kwa ndani ilikuwa na vitu vingi vya thamani kubwa.Tuliingia mpaka sitroom na kupumzika kidogo.Walikuja vijana wawili na kusalimiana na sisi kisha wakaingia chumba kingine.
“Nisubiri hapa kwa robo saa,sawa?”Yule mchungaji aliniambia nimsubiri.Aliinuka na kuingia kile chumba walichoingia wale vijana waliotusalimia pale sitroom.
Nilianza kuingiwa woga baada ya kusikia sauti za ajabu ajabu zikilia mle chumbani.Nilipata ujasiri kidogo wa kusogea hadi karibu na mlango.Mara nikaanza kusikia.
“Warionka warionka of God is able.”sauti niliyoisikia ikitamka maneno hayo ni ya yule mchungaji niliyefuatana naye.
“Where is sacrify?”sauti nyingine ya kutisha ilisikika ikihoji.
“I will bring here tomorrow morning,don’t worry my great God.”pia nilisikia nyimbo za ajabu ajabu zisizoeleweka zikiimbwa ndani ya chumba kile.
Nilirudi haraka na kuketi juu ya sofa.Baada ya dakika 15 nilishuhudia watu zaidi ya hamsini wakitoka ndani ya chumba kile kile alichoingia mchungaji.Wengi wao walikuwa wamechafuka damu midomoni na mikononi.Niliogopa sana lakini cha kushangaza hata mtu mmoja hakunisemesha.Walitoka nje na kutokomea pasipojulikana.Haukupita muda mrefu yule mchungaji naye alitoka kama wale wengine,pia alikuwa amechafuka damu nyingi sana.

***************
Je nini kitatokea baada ya Mr.Cheo kumwona mchungaji akiwa amechafuka damu nyingi baada ya kutoka mule chumbani aliposikia sauti za ajabu na nyimbo zisizoeleweka.....?Usikose sehemu inayofuata.
 
MTUNZI-FREDY MZIRAY

No comments:

Post a Comment