Jina la Flora Lyimo au Mbuta Nanga limekuwa maarufu katika mitaa ya Oxford inayosifika kwa kuwa na wabunifu wakubwa duniani, jijini London nchini Uingereza.
Hata hivyo, hakuna anayejua ukweli kuhusu historia ya maisha ya Mbuta Nanga, Mtanzania ambaye kwa sasa ni raia halali wa nchi hiyo. Flora anayemiliki duka kubwa la mavazi katika mitaa hiyo, amekuwa kivutio kikubwa kwa wengi wanaohitaji mavazi ya kibunifu, hasa kutokana na ucheshi, pamoja na uzoefu wa kufanya biashara hiyo kwa muda mrefu.
Haikuwa rahisi kwake kufikia hatua hiyo kwani historia yake inaonyesha kwamba, Mbuta Nanga hakubahatika kusoma kutokana na wazazi wake kutokuwa na uwezo. Binafsi anasema kuwa mafanikio aliyonayo sasa ameyatafuta kwa miaka 30 hadi kuyafikia.
Katika mahojiano na gazeti hili, dada huyo anasema kuwa, hakuridhika na hali halisi ya kimaisha, hivyo alianza kufikiria namna atakavyoweza kujiimarisha ili aipe furaha familia baada ya kumaliza darasa la saba.
Mwaka 1989 Kijijini Kilema Marangu
Huku ndiko maisha ya Flora (Mbuta Nanga) yalikoanzia.
Anasema kuwa baada ya kuhitimu elimu ya msingi, hakufanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari hivyo elimu yake ni darasa la saba mpaka sasa.
“Nimezaliwa katika Kijiji cha Kilema huko Marangu, Moshi Kilimanjaro Aprili 23, 1974 katika familia ya Basilei Pius Lyimo na Augustina Lyimo. Tumezaliwa watoto 11, wasichana saba na wavulana watatu, mimi nikiwa mtoto wao wa saba ‘lucky seve’ kama nilivyokuta wakisema Waingereza,” anaanza kusimulia.
Anasema kuwa baada ya kukamilika kwa muda wa kuanza shule, alisoma katika Shule ya Msingi Kilema Kubwa mpaka darasa la saba na kufanikiwa kuhitimu mwaka 1989.
“Nasikitika kwani hapo ndipo elimu yangu ilipoishia, kwa kuwa wazazi wangu hawakuwa na uwezo wakunisomesha sekondari, japo nilitamani sana kuendelea na masomo,” anasema.
Mbuta Nanga anasema kuwa hakuwa na namna bali kujiandaa kwenda mjini kutafuta kazi ili arudi nyumbani kila Sikukuu ya Krisimasi arudi nyumbani na mabegi makubwa ya zawadi kama ulivyo utamaduni wa watu wa Kabila la Wachaga tangu enzi hizo mpaka sasa.
“Kama nilivyokuwa naona watu wakija kijijini wakati wa Krisimasi na mabegi nilidhani ilikuwa ni kazi rahisi. Nilifikiri kwenda mjini inaimanisha kila Krisimasi ni kurudi kijijini na zawadi kibao, kumbe wapi, kuwa ujionee,” anasema.
Anasema kwamba alitamani kusoma lakini hakuwa na jinsi bali aliamua kutulia kwanza nyumbani mpaka atakapopata bahati ya kutoka. “Kwa kuwa nilikuwa na kiu ya pesa, nilihisi ipo siku nitamiliki pesa nyingi kama nitajituma na hilo hasa lilikuwa lengo langu,” anasema Mbuta Nanga.
Anafafanua: “Basi mwaka 1990 nilibahatika kwenda mjini kwa mara ya kwanza, nilichukuliwa kijijini kwetu kwenda kufanya kazi za ndani hasa kukaa na mtoto wa dada mmoja naye ni Mchaga, aliyekuwa akiishi Nairobi. Alimwambia mama yangu kwamba nitakuwa namwangalia mtoto wake mmoja aliyekuwa naye wakati anakwenda kazini na akirudi jioni mimi nitakuwa naenda shule kujifunza kizungu na kuandika kwa mashine (computer).”
Anabainisha kuwa haikuwa rahisi kwa mama yake kukubali ombi hilo, lakini aliposhawishiwa zaidi alimkubalia na kumwachilia aende Nairobi kutafuta maisha.
“Mama yangu akakubali, ndipo safari yangu ya Nairobi ikaiva. Nilikaa Nairobi kwa mwaka mzima na ilipofika Desemba 1990, wakati wa Sikukuu ya Krisimasi, nikarudi nyumbani. Kabla ya safari, yule dada alinikataza kununua vitu na kuniambia nipeleke pesa nyumbani, kwani zitamsaidia mama kwa kuwa sijui anashida gani. Ni mwaka sasa sijamwona yeye na ndugu zangu hivyo ni vizuri kwenda na pesa,” anasema.
Anasimulia kuwa kutokana na kuhisi ushauri huo unafaa, alikubaliana naye kwa shingo upande ili kumridhisha.
“Nilimsikiliza na nikaenda na kibegi kimoja ambacho sikupenda kwa kweli, lakini tulienda kufanya shopping za kila kitu nikiwa na mama yangu na ndugu zangu wote walikuwa na furaha kweli, sikukuu ilipokwisha nilirudi tena Nairobi kwa yule dada na nikaendelea na kazi za nyumbani. Kazi yangu ilikuwa ni kukaa na mtoto wake na kweli jioni nikaenda shule kujifunza Kiingereza na kuandika kwa kompyuta,” anasema.
Kunyanyaswa kijinsia
Mwaka 1991 wakati huo (Flora) akiwa na umri wa miaka 16 na alishaanza kubadilika kimaumbile na kuona mambo mengi ya mjini, hasa kuhusu ujana lakini hakujishughulisha nayo.
“Nilianza kupata shida kwa mume wa yule mama. Kila anapopata nafasi alikuwa akirudi nyumbani bila mkewe na kunikuta, kisha kunipapasa na kutaka nifanye naye mapenzi. Mimi nilimkatalia, lakini unyanyasaji huo ulikuwa unaniumiza moyoni hata nikalia sana,” anasema.
Mbuta Nanga anasema kulia kwake hakukumsaidia kwani jamaa huyo aliendelea kumnyanyasa kwa kumtaka kimapenzi jambo ambalo hakuwa tayari na alihisi hakustahili.
“Niliwahi kumwambia kwamba ningemweleza dada, hapo akaniomba nisimwambie akaahidi hatofanya tena. Tatizo lilikuwa kwamba kila usiku anapokuja mimi ndiyo huenda kufungua mlango na dada (mke wake), anakuwa amelala.
Alikuwa hamfungulii mlango sababu mumewe alikuwa mlevi sana. Hivyo kila akirudi amelewa na hapo huanza kugombana, basi akanipa mimi hiyo kazi ya kumfungulia mlango,” anasema.
“Kila akiingia alikuwa akianza kunishika matiti na huku anataka kunibusu, basi kimya kimya nikawa namtoa mikono na kujizuia ili dada asisikie kwani sikupenda mimi niwe chanzo cha ugomvi wao, nilipoona anaendelea hivyo nikamwambia mama mmoja rafiki wa dada. Dada akaamua kuniondoa pale na kwenda kukaa na huyu mama rafiki yake, huku nikawa naendelea na shule,” anasema na kuongeza:
“Kwa yule mama mwingine, yeye alikuwa na mume ila hana mtoto. Basi nikawa naenda kanisani kila Jumapili nilikuwa mapumzikoni. Huko kanisani nilikutana na akinadada wafanyakazi za nyumbani kama mimi, tukawa tunaongea na kufahamiana. Wengi walikuwa Watanzania,” anasimulia.
Mbuta Nanga anasema kwa kipindi kile Kenya kulikuwa na sheria ya kila mtu kuwa na kitambulisho cha makazi na cha uraia, lakini upande wake hali ilikuwa tofauti.
Chakacha yamharibia ajira
Kama una kumbukumbu mwanzoni mpaka mwishoni mwa miaka ya 1990, uchezaji wa chakacha ulikuwa miongoni mwa mitindo ya kipindi hicho, iliyoteka hadhira na safari hii Mbuta Nanga alishawishiwa kuingia huko.
Anasema kuwa Jumapili moja alikutana na binti mwingine ambaye alimshawishi waende wakaangalie shoo sehemu moja jijini Nairobi.
“Basi tukaenda naye kulikuwa na msichana mmoja alikuwa anacheza chakacha na nilipoona anavyocheza nilifurahi na kusema hata mimi nitaweza. Yule msichana akaniambia kama nitaweza basi niende kucheze, niachane na kazi za nyumbani.
Tukaenda mimi na yeye na kuuliza mtu akitaka kucheza kama yule dada wa chakacha anahitaji nini, tukaambiwa ni wewe uje mchana utuonyeshe jinsi unavyocheza halafu tutakuambia kama unaweza au la,” anasimulia
Mbuta Nanga anasema kuwa haikuwa rahisi kwake, lakini alimwomba kwenda siku ya Jumapili, ndipo anapopata nafasi na kukubaliwa kutoka.
Itaendelea wiki ijayo
chanzo:mwananchi
Itaendelea wiki ijayo
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment