Friday, 21 November 2014

Mwanafunzi Kidato cha kwanza abakwa darasani

                                           Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Carren Yunus

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza A katika shule ya sekondari Ntunduru wilayani Sengerema mkoani Mwanza (jina limehifadhiwa, 14), amejeruhiwa vibaya sehemu za siri na shingoni kutokana na kukabwa shingoni wakati akibakwa ndani ya chumba cha darasa la shule hiyo mchana.

Tukio hilo lilitokea Novemba 15, mwaka huu mchana huku baadhi ya walimu wakidaiwa kuwapo shuleni baada ya mwanafunzi huyo kuitwa na mhitimu wa kidato cha nne ambaye anatuhumiwa kutenda kosa hilo.

Mwanafunzi huyo baada ya kuingia katika darasa hilo, alikutana na wanafunzi wawili wa kidato cha nne waliomkaba shingo na kumziba mdomo kisha kumvua nguo na kuanza kumtendea ukatili huo.

Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Carren Yunus, alisema watuhumiwa hao lazima wapatikane na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Pamoja kuwasaka watuhumiwa pia lazima ufanyike uchunguzi wa kina juu ya usalama wa wanafunzi wa  kike katika shule hii binafsi mchanganyiko ya bweni,” alisema Yunus.

Makamu mkuu wa shule hiyo, Bahati Charles, alithibitisha kutokea kwa tukio na tayari wanafanyia uchunguzi pamoja na vyombo vya dola.
“Ni kweli tukio hilo limetokea, ni tabia tu ya vijana wa leo kukosa maadili,” alisema Charles.

Polisi wilayani Sengerema imethibitisha kuwapo tukio hilo lenye jalada Seng/RB/2949/2014 ya Novemba 15, na kuwataja watuhumiwa ambao hata hivyo majina yao yanahifadhiwa.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Valentino Mlolowa, alithibitisha kutokea kwa tukio na hilo na kusema msako wa wahusika unaendelea.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment