Thursday 20 November 2014

Ulimuacha mke, sasa unataka akurudie kama kimada!


Zipo familia ambazo hujikuta kwenye mitafaruku ya kifamilia kiasi cha kusababisha mama kuondoka kwenda kujitafutia maisha kwingine. Inawezekana mitafaruku ikasababishwa na mume mwenyewe kumnyanyasa mkewe au mama mkwe kuwa chanzo.

Mume aweza kuwa amepata mwanamke mwingine nje ya ndoa hivyo kumnyanyasa mkewe wa ndoa ili kumfanya aghadhabike na kujiondokea zake.

Inapotokea hivyo, wapo baadhi ya kinababa hufurahia ili huyo mwingine azibe nafasi. Huu ni usaliti ambao hata Mungu haupendi.

Mwingine anafiwa na mkewe lakini hapo kabla tayari alikuwa na mwanamke nje ya ndoa na watoto aliozaa na mkewe anawatelekeza. Je, nini kinatokea baada ya hapo?

Nitakupa mifano miwili inayodhihirisha matukio ya hicho ninachojaribu kuonyesha hapo juu.

Kwanza nianze na mume aliyeacha mke. Juzi nikiwa nasikiliza Redio moja alfajiri, msikiliza mmoja akamuuliza mtangazaji, je, ni haki?

Yupo jamaa mmoja alimuacha mkewe na kwenda kuoa mwanamke mwingine, huko mambo yakamchachia akamrudia mkewe wa mwanzo na kumuomba warudiane lakini kama kimada wake.

Mpenzi msomaji, alipotamka hilo la kimada nikajikuta nimecheka kwa sauti kubwa na mtangazaji naye akacheka. Yaani kwa mtu yoyote aliyesikia maneno yale ni lazima acheke. Ulimuacha, sasa umedata unataka awe kimada wako? Jamani!  Ama kweli Maisha ndivyo Yalivyo.

Hicho ni kituko cha kwanza. Hiki kingine ndio babu kubwa. Yupo jamaa alifiwa na mkewe. Lakini kabla ya kifo walikuwa wametengana ambapo kila mmoja alikwenda kujinafasi kivyake. Huyu akaoa na yule akaolewa kwingine.

Kabla ya kufarakana tayari walikuwa na watoto wakubwa watatu, mkubwa akiwa tayari ameanza kujitegemea na ameshaweza kujenga nyumba yake ndogo ya vyumba viwili.

Pale msibani ndipo mambo yakabumburuka. Kwanza muda mwingi baba wa watoto hao alikuwa muda mwingi kajiinamia akionekana kuwa na mawazo mazito.

Inawezekana alikuwa akijaribu kutafakari maisha yalivyokuwa kati yake na marehemu yalivyokuwa wakati wa uhai wake na jinsi ambavyo mwisho ulivyokuwa mbaya ambapo hakuweza hata kumzika mkewe kijijini kwake na badala yake akazikwa hapa Dar.

Ajabu hata mama mkwe hakuja kwenye mazishi, jambo ambalo liliwashangaza wengi.
Kwenye kikao pale msibani watoto walihoji mbona baba yao aliwatelekeza kwa takriban miaka minane bila kujua wanaishi vipi. Wakahoji hata kama alikuwa na mwanamke mwingine mbona hajawatambulisha wamjue?

Baba yao akajing’ata ngata akijitetea kuwa hajawatelekeza na kwamba anawapenda sana. Akaambiwa na wajumbe wa kikao cha familia kwamba anatakiwa akafanyiwe usuluhishi nyumbani kijijini kupatanishwa na watoto wake.

Hata hivyo watoto wakaibua dai lingine wakitaka baba yao kama kweli anawakubali ni watoto wake aje ahame kwa huyo mwanamke aje akae nao.

Yule mtoto mkubwa(wa kiume) mwenye nyumba akamwambia baba yake anamruhusu aje akae hapo nyumbani lakini siyo na huyo mwanamke(wajumbe wa kikao wakaangua kicheko).

Mtoto mwingine wa kike akainuka na kusema kama baba yao hataki kuja kuishi nao, basi baba yao apange zamu ya kukaa nao yaani kama wiki hii ataishi nao basi wiki ijayo akaishi na huyo mkewe mwingine(wajumbe wa kikao wakaangua tena kicheko).

Mpenzi msomaji, ijapokuwa  kilikuwa ni kikao cha kuanua tanga ambacho nami nilishiriki, ilikuwa ni burudani ya aina fulani. Kwa ujumla baba yule alipata aibu kubwa.

 Kwa baba anayeithamini familia yake na kuwajibika vilivyo, hakupaswa kuwasahau watoto wake hata kama ametengana na mama yao. Alipaswa kuwa karibu nao kwani ndiyo baraka na hazina aliyompa Mwenyezi Mungu.

Angalia mke aliyemzalia watoto wazuri, wenye akili ambapo mkubwa ameweza kujenga nyumba yake ambako ndiko walikokuwa wakimuuguzia mama yao, na baba mwenyewe hajaweza hata kuwa na kibanda, amepangisha.

Mtoto huyo mkubwa wa kiume alitamka wazi kuwa yuko radhi kumwachia baba yake nyumba ile ikiwa atarudi kuishi hapo lakini kwa sharti kwamba asimlete pale mwanamke wake huyo. Sharti hilo baba huyo alilikataa kwa madai eti tayari amezaa na mwanamke huyo hivyo hawezi kukaa mbali naye.

Hata ile ofa ya kuja kukaa na wanawe kwa wiki kisha aende tena kwa mkewe huyo hakuiafiki. Kikao kikaamua kuwa majibu zaidi ya maswali hayo yatapatikana wakati watoto hao watakapokwenda kijijini ambako kikao cha ukoo kitafanyika.

Mpenzi msomaji, hayo ndiyo mambo ndani ya nyingi ya familia. Usione watu barabarani wakitabasamu kumbe wamebeba mizigo mizito vichwani na nafsini mwao. Hakika Maisha Ndivyo Yalivyo
chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment