Monday, 5 January 2015

Panya Road 36 washikiliwa na polisi

Jeshi la  Polisi  linawashikilia watuhumiwa  36 wa kundi la vijana wanaojiita   ‘panya road’  ambao hupita mitaani au  barabarani  jijini Dar es Salaam kushambulia, kujeruhi na kupora watu wakitumia silaha mbalimbali.

Vijana hao wanadaiwa kufanya uhalifu kwa kutumia  nondo, mikuki, mapanga,  fimbo, visu na kutukana matusi ovyo.

Watu hao wanashikiliwa siku moja, baada ya wakazi wa  Dar es Salaam kukumbwa na taharuki, kufuatia  kikundi cha ‘panya road’ kupita maeneo tofauti kwa lengo la kufanya fujo ikiwa ni pamoja na kupora na kujeruhi.

Kikundi hicho kilichafua hali ya hewa kwa madai kuwa, mwenzao  Mohamed Ayubu mkazi wa Tandale kwa Mtogole ambaye alituhumiwa kuwa mwizi kuuawa na wananchi mkesha wa kuamkia mwaka mpya na kuchomwa moto.


Kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi la Polisi , Advera Bulimba,  vijana walioko mahabusi wana umri kati ya miaka 16 na  30 ambao wanaendelea kuhojiwa na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Bulimba alisema wakati wakiendelea na mahojiano na watu hao, wameagiza makamanda wa polisi kote nchini, kuhakikisha makundi ya watu hatari kwenye jamii yanakamatwa.

“Jeshi limejipanga vya kutosha kuhakikisha nchi inaongozwa kwa kufuata utawala wa sheria, hatutamwonea muhali mtu yeyote ama kikundi cha watu wanaotaka kuvuruga amani na kutia hofu wananchi,” alisema.

Aliongeza kuwa, kabla ya tukio hilo kutokea walipata taarifa za  kuwapo kwa watu hao ambao walijipanga kufanya fujo mara baada ya kumzika mwenzao  na kujiimarisha kwa kuongeza ulinzi kila mahali ili kuwadhibiti.

Alisema kundi hilo ambalo lilikuwa ni rafiki za marehemu, mara baada ya kumzika mwenzao makaburi ya Kihatu Kagera Mikoroshini, lilianza kutawanyika na kuanza kufanya fujo.

Aliwaambia wanahabari kuwa jeshi la polisi liliwadhibiti kwa kupiga mabomu ya machozi ambayo yaliwatawanya.

“Wananchi walipatwa na hofu wakidhani kuwa huko walikokimbilia wataendeleza vitendo vya kihalifu, lakini polisi tayari walikuwa wamezagaa kila kona kudhibiti hilo,” alisema.

MFADHILI ANASAKWA
Bulimba alisema kwa sasa wanaendelea kuchunguza ili kumbaini mfadhili wa kundi hilo na yale mengine ambayo yamekuwa tishio mitaani.

Aidha  ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa kupiga simu namba 0754785557 ya Mkuu wa Jeshi  au za makamanda wa polisi wa mikoa ili kuyaibua makundi hayo.

Pia jeshi hilo limewataka wazazi kuwa makini na watoto wao hasa wale wanaotoka nyakati za usiku kwa kuhakikisha wanafuatilia mienendo yao.
Kuhusu uharibifu wa mali na athari kwa wananchi, jeshi hilo limesema hadi jana halijapokea malalamiko yoyote kutoka kwenye jamii.

Fujo za kundi hilo lilisababisha baadhi ya wananchi kujifungia majumbani huku wengine wakishindwa kurudi nyumbani kwa hofu ya kupoteza  maisha yao.

SEHEMU ZILIZOATHIRIKA

Maeneo ambayo yalikumbwa na taharuki hiyo iliyoanza jioni juzi ni pamoja na Buruguni, Mwananyamala, Tandale, Sinza, Kinondoni, Kigogo, Tabata na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Shuhuda wa tukio hilo, Amina Said mkazi wa Tandale alisema kuwa, kundi hilo lilianza kupora watu maeneo ya Tandale kwa Tumbo wakiifuata barabara ya Makanya kuelekea maeneo ya Sinza.

Mmoja wa wafanyabiashara eneo la Magomeni ambaye aliyejitambulisha kwa jina moja Nathan alisema kuwa waliwaona wakiwa na silaha tofauti yakiwemo mapanga ndipo walipolijulisha jeshi la polisi.

Alisema baada ya mazishi ya mwenzao, jeshi la polisi lilifika na kuwatawanya kwa kupiga mabomu.

Alisema hali hiyo ilisababisha wafanyabiashara kufunga biashara zao kwa kuhofia kuibiwa au kujeruhiwa na kundi hilo.

"Nimekuja hapa kituoni kumchukua mke wangu na watoto nimesikia kuna Panya Road ambao ni hatari, nimewasiliana nao nashukuru Mungu wote wapo salama," alisema Digonzo mkazi wa Mwananyamala.

Aidha, wananchi wameonyesha kushangazwa na kauli ya Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova, aliyoitoa kwenye vyombo vya habari kuwa, hakuna tukio hilo.

Mkazi wa Mwananyamala, Said Hassan alisema kauli hiyo imewavunja moyo kwa kuwa, walishuhudia kundi hilo la ‘panya Road’  wakiwa wanafanya fujo na kuiba na kusababisha taharuki.

"Taarifa hizi ni za kweli na siyo za kizushi kama alivyodai kamanda Kova na kwamba panya road hao wanatakiwa kudhibitiwa kwa haraka," alisema.

Chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment