Friday 15 November 2013

Bastola ya marehemu Dk. Mvungi yakamatwa, bado kompyuta

Wakati mwili wa aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, ukiwasili kesho nchini, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limetangaza kumkamata mtuhumiwa mwingine aliyehusika katika tukio la kumvamia, kupora na kumjeruhi, nyumbani kwake Novemba 03, mwaka huu akiwa na bastola iliyoibwa kwa marehemu.

Idadi hiyo inakamilisha watuhumiwa 10, ambao mpaka sasa wanashilikiwa na Jeshi la Polisi kwa kuhusika na tukio hilo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alimtaja mtumhumiwa huyo kuwa ni John Mayunga (56), maarufu kwa jina la Ngosha, mkazi wa Kiwalani, wilayani Temeke.

Kova alisema mtuhumiwa alikamatwa kwa msaada wa raia mwema ambaye alisaidia kutoa taarifa.

“Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia mwema juzi, kwamba kuna mtu amehusika na tukio la Dk. Mvungi  ameonekana katika mtaa wa Twiga Jangwani akiwa anaangalia televisheni, baada ya kupata taarifa hizo walikwenda na kumkamata,” alisema Kova na kuongeza:

 “Baada ya kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake, mtuhumiwa huyo alikutwa na bastola aina ya Revolver No. BDN 6111 pamoja na risasi 21 ambayo iligundulika kuwa ni mali ya Dk. Mvungi pamoja na baruti aina ya Explogel yenye muundo wa Sausage, Tambi mbili ambazo ni viwashio vya baruti (Detonator) na mingine minne ambayo ilikuwa imeunganishwa tayari kwa kutumika.”

Kova alidai mtuhumiwa alikiri kuhusika katika tukio la kumjeruhi na kumpora Dk. Mvungi kwa kushirikiana na wenzake ambao tayari wamekamatwa na kwamba amewahi kutumikia kifungo kwa miaka saba.


Pia, Kova alisema bado wanaendelea na upelelezi ili kuhakikisha komputya mpakato (Laptop) inapatikana pamoja na simu moja ambavyo ndivyo vimebaki.

Alisema mpaka sasa wako katika hatua nzuri ya kukamilisha upelelezi wa kupatikana vitu hivyo.

“Upelelezi wetu kwa sasa umefikia asilimia 90 kwa sababu karibu vitu vyote vimeshakamatwa, kilichobaki na kama watuhumiwa wawili tu; wa simu na wa laptop,” alisema Kova.

Novemba 11, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, waliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza hatua za upelelezi wa tukio hilo zilipofikiwa.

Hata hivyo, hawakueleza upelelezi wa kompyuta hiyo umefikia wapi kwa madai wanaendelea kuitafuta.

Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, upelelezi umekamilika kwa asilimia 80 na umefanywa kwa umakini mkubwa kuhakikisha waliotenda tukio hilo wanatiwa kwenye mikono ya sheria.

Kamanda Kova aliwataja watuhumiwa tisa waliokamatwa wakiwa na mapanga matano na simu aina ya Nokia iliyokuwa inatumika nyumbani kwa Dk. Mvungi, huku mmoja wa watuhumiwa akiwa ni fundi ujenzi wa nyumbani humo.

Dk. Mvungi ambaye alikuwa mwanasheria mkongwe aliyebobea katika masuala ya sheria na Katiba, alihamishiwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi lakini alifariki dunia juzi.

Kuna hisia kwa baadhi ya watu kwamba huenda alivamiwa nyumbani kwake kwa hisia kuwa wajumbe wa tume hiyo wanalipwa fedha nyingi na hivyo kulikuwa na uwezekano wa kuwa na fedha nyingi nyumbani kwake.

Hata hivyo, pamoja na hisia hizo, pia kuna hofu miongoni mwa jamii kuwa huenda alijeruhiwa na kuporwa laptop yake ambayo ilikuwa na taarifa muhimu na nyeti kuhusu mchakato mzima wa Katiba Mpya na taarifa hizo zitakuwa mikononi mwa watu wasiostahili.

Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba miongoni mwa vitu vilivyoporwa nyumbani kwa Dk. Mvungi, baada ya kupigwa mapanga na majambazi hao ni laptop ambayo ni moja ya nyenzo zake muhimu za kazi.

Hofu hii inaelezwa kutanda ndani ya Tume kuwa mbali ya kuwako na uwezekano huo, kwa kuwa Dk. Mvungi amebobea katika masuala ya Katiba, alikuwa nguzo muhimu kwa Tume hasa katika kipindi hiki cha mwisho cha kuandaa rasimu ya mwisho ya Katiba Mpya
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment