Thursday, 20 November 2014

Kenya, India zaipiku Tanzania mauzo ya tanzanite




Arusha. Nchi za Kenya na India zimeipita kwa mbali Tanzania kwa kusafirisha na kuuza katika soko la dunia, madini ya tanzanite ambayo yanapatikana hapa nchini pekee.

Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa jana kwamba kwa mwaka jana, Tanzania haikufikia hata nusu ya Kenya kwa mauzo ya madini hayo ya vito.

Kamishna Masanja alisema mwaka jana pekee, Kenya ilisafirisha na kuuza nje ya nchi tanzanite yenye thamani ya zaidi ya Dola 100 milioni za Marekani (Sh173 bilioni) dhidi ya Dola 38 milioni (Sh45.5 bilioni) zilizouzwa na Tanzania.

“Katika kipindi hicho cha mwaka jana, India iliuza tanzanite zenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani 300 milioni (Sh509 bilioni) kiasi cha baadhi ya wanunuzi wakubwa, hasa kutoka Marekani kujiuliza iwapo madini hayo yanachimbwa India,” alisema Masanja.

Bila kumtaja jina, Kamishna huyo alisema mmoja wa wanunuzi wakubwa wa madini ya vito kutoka nchini Marekani aliwahi kumuuliza iwapo kuna migodi ya tanzanite India kwa sababu akifika huko hupata tanzanite bora na zenye ukubwa kuliko anayopata Tanzania.

Alisema zaidi ya asilimia 80 ya tanzanite inayopatikana Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, Manyara huuzwa kwa njia za panya nje ya nchi na kwamba Serikali imeanza kuchukua hatua.

“Serikali inakusudia kuunda kikosi kazi kitakachojumuisha askari kutoka vyombo vyote vya ulinzi na usalama kukabiliana na utoroshaji madini nje ya nchi.”

Alisema hivi karibuni, wizara itawasilisha muswada bungeni kurekebisha Sheria ya Madini Namba 6 ili kumpa mamlaka Kamishna wa Madini kutaifisha madini yote yanayokamatwa yakisafirishwa kinyume cha sheria.

“Tunataka sheria ya madini ifanane na ile ya misitu inayotaifisha mazao yote ya misitu yanayovunwa kinyume cha sheria, tofauti na sasa ambapo tunalazimika kusubiri uamuzi wa Mahakama kutaifisha madini iwapo watuhumiwa wanatiwa hatiani,” alisema.

Hadi sasa, Serikali imekamata na kutaifisha madini yenye thamani ya zaidi ya Sh15 bilioni yaliyokamatwa yakitoroshwa nje ya nchi baada ya watuhumiwa kutiwa hatiani na Mahakama.

“Tuna mpango wa kujenga kituo maalumu cha madini kitakachojulikana kama Madini House kitakachokuwa na ofisi zote za kununua na kuuza madini ya vito ili kudhibiti biashara holela,” alisema Masanja.

Alisema katika kituo hicho kutakuwa na huduma za kodi na malipo mbalimbali ya Serikali pamoja na usafiri wa helikopta za kusafisha madini kwenda viwanja vya ndege ili kuepuka wizi na uvamizi njiani
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ngosi Mwihava  aliwataka Watanzania kushiriki katika vita dhidi ya uhujumu uchumi na kwamba juhudi za Serikali za kupambana na wanaotorosha madini nje ya nchi haziwezi kufanikiwa bila ushiriki wa umma kwa kutoa taarifa kwa vyombo na mamlaka husika.
chanzo:mwananchi
 

No comments:

Post a Comment