Monday 24 November 2014

Ni aibu Kenya, India kuuza Tanzanite nyingi


SI jambo la kufurahia hata kidogo taarifa za Kenya na India kuizidi Tanzania katika mauzo ya vito aina ya Tanzanite nje ya nchi.
Tunasema si jambo la kufurahia kwakuwa Tanzania ndiyo mzalishaji pekee wa madini ya vito hivyo katika hali ya kawaida ndiyo ingetakiwa iwe kinara wa kuuza bidhaa hiyo.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja, India ndiyo inayoongoza kwa biashara ya Tanzanite duniani.
Mwaka jana pekee nchi hiyo iliuza nje Tanzanite yenye thamani ya sh bilioni 509 ikifuatiwa na Kenya iliyouza nje Tanzanite yenye thamani ya sh bilioni 173 huku Tanzania ikiuza Tanzanite yenye thamani ya sh bilioni 5.5
Takwimu hizi si tu hazifurahishi masikioni mwa Watanzania lakini zinahatarisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kutokana na kupoteza mapato mengi yapatikanayo kwenye Tanzanite.
Tunajua Kenya na India zinauza Tanzanite nyingi zaidi kuliko Tanzania kwakuwa zimejiandaa kikamilifu kwa kuanzisha viwanda vya kuchakata madini hayo tofauti na Tanzania.
Kwa muda mrefu serikali imekuwa ikitoa ahadi za kuanzisha viwanda vya uchakataji wa madini hayo hapa nchi ili kuyaongezea thamani lakini mpaka hivi sasa jambo hilo halijapatiwa uzito unaostahili.
Tunaamini serikali inapaswa ilivalie njuga suala hili ili kuongeza mapato yake badala ya kila kukicha kubisha hodi kwa nchi wahisani na wafadhili kuomba fedha za kusaidia bajeti.
Zipo taarifa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Tanzanite inayozalishwa Mererani mkoani Manyara, hutoroshwa nje ya nchi kwa njia za panya lakini mpaka sasa serikali haijadhibiti utoroshwaji huo.
Ni aibu kusikia inakusudia kuunda kikosi kazi kitakachojumuisha askari kutoka vyombo vyote vya ulinzi na usalama kukabiliana na utoroshaji madini nje ya nchi badala ya kuimarisha au kuanzisha viwanda vya kuchakata madini hayo.
Tunaamini serikali inakosa fedha nyingi kwasababu ya ukosefu wa ubunifu wa kuziba mianya ya biashara za magendo, holela na ukwepaji kodi unaofanywa na watu wachache.
Soko la ajira Tanzania litaongezeka kama serikali itawekeza kwenye uchakataji wa Tanzanite, tukiruhusu India na Kenya ziendelee kuuza kwa wingi madini hayo tutaendelea kushuhudia maendeleo ya kiuchumi kwenye nchi hizo.
Ni aibu kila kukicha serikali kufikiria kuwabana wananchi na wafanyakazi katika kodi huku ikiacha mianya ya utoroshwaji wa Tanzanite na madini mengineyo.
Tunaamini serikali na watendaji wake wanapaswa kuacha kufanya kazi kwa mazoea, urasimu au uzembe ili nchi iwe na mapato mengi yatakayosaidia kukuza pato la taifa.
Tungependa takwimu za India na Kenya kuuza Tanzanite nyingi kuliko Tanzania iwe chachu kwa viongozi wetu kubuni mbinu za kuchakata madini hayo hapa nchini pamoja na kuminya mianya ya utoroshwaji wake.
Chanzo:TzDaima

No comments:

Post a Comment