Monday, 1 December 2014

Kwanini mama awafundishe watoto kumdharau baba yao?

Anacholalamika baba huyo katika ujumbe wake ni kwamba, ni kwanini mkewe awafundishe watoto wao wamdharau kwa kuwa mama ana kipato? Hivi jambo hilo lilistahili kuhusishwa watoto kwa namna ya kumdhau baba yao?

Nadhani mama huyu hakumtendea haki kabisa mumewe wala watoto wao. Zipo nyumba nyingi tu ambazo baba kipato chake ni cha chini huku kile cha mkewe ni kikubwa lakini wanaheshimiana.

Na zipo nyumba ambako kipato kikubwa cha mama kilitokana na kuinuliwa kiuchumi na mumewe. Inawezekana mumewe ndiye aliyemwanzishia mradi/miradi au kumsomesha hata kuweza kupata ajira katika nafasi ya juu.

Sasa kinamama waliowezeshwa na waume zao kwa njia hii wanathubutuje kudharau waume zao? Hii siyo haki kabisa.

 Ndipo nikayafurahia maandiko matakatifu hapo juu kwamba “  mwanamke atamlinda mwanamume”.  Na pia kwamba “Mwanamke mwema ni taji la mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake”.

Sasa mpenzi msomaji wangu, mwanamke huyo anayewafundisha watoto kumdharau baba yao anamlinda vipi mumewe kama siyo kumwaibisha mbele za watoto?

Watoto nao wamehimizwa kuwatii wazazi wao ili wapate heri na maisha marefu. Sasa mama huyu anayewafundisha kumdharau baba yao na kuwaondolea utii kwa baba yao, maisha marefu watoto hawa watayapata wapi? Na mama huyu ana tofauti gani na maneno ya kibiblia yanayomfananisha na ‘kuoza mifupani mwake’.

Mwanamke anapaswa kumlinda mumewe. Hata kama anafanya vituko vya sayari nyingine, anapaswa kuwa makini katika kutafuta chanzo na siyo kumdhalilisha, kumwaibisha mbele ya watoto na hata jamii kwa jumla.

Labda niulize; kwani kama mume huyu ana kipato kidogo, mke huyu si alimpenda pamoja na mapungufu hayo?

Hawa walikubaliana kuishi pamoja kwa raha na taabu. Iweje leo mama kipato kimepanda aanze kumdharau mumewe? Mwanamke ndiye anayetoka kwa wazazi wake na kuolewa.

Mwanaume ndiye anayemzungumzia maneno mazuri mwanamke ili kumshawishi ampende. Mwishowe wanakubaliana kuoana, hivyo mwanamke anawaacha wazazi wake anaatambatana na mwanaume, wanaoana.

Sasa mwanaume aliyekutoa kwenu, akakulipia mahari, ukaonyesha unyenyekevu wa hali ya juu, sasa wamezaliwa watoto ambao ndio baraka ya ndoa, unaanza dharau kwa kuwafundisha watoto nao wamdharau baba yao. Ni sawa hii? HAPANA.

Yapo mambo ambayo mwanamke anapaswa kuyahifadhi na kuyalinda mapungufu au madhaifu ya mumewe. Mwanamke anayefanya kinyume na hili anafanya kufuru mbele ya Mwenyezi Mungu.

Familia ni baba, mama na watoto. Wazazi hawa wana nafasi kubwa katika familia. Wao ndio wanaijenga kwa njia mbalimbali, na umoja wao ndio utakaofanikisha kuwa na familia bora hasa kwa kuzingatia yafuatayo:
• Kwa kutoa na kuhakikisha familia ina mahitaji muhimu kama chakula, malazi, mavazi na elimu

Baba akiwa ndio kichwa cha familia na mama akiwa nguzo ya familia.
Tumeona jinsi mama anavyowajibika kuhakikisha baba anapata support kubwa sana kutoka kwake na kuwa mshauri mkubwa katika kuhakikisha familia inakua sawa, mama huyo huyo anahakikisha mazingira ya nyumba yapo safi na mahitaji yote ya nyumbani yapo kwa wakati, kupika, kufua, kuhakikisha watoto wamekula, kupasi n.k ndio maana nasema mama ni nguzo ya familia.

• Kuwasikiliza watoto kwa kuwapa ushauri na kutatua matatizo yao.
• Kutoa upendo wa kweli kwa watoto wao bila upendeleo.

• Kuwapa watoto nafasi ya kucheza, kulala kusoma na kujifunza shughuli mbalimbali.Tutambue kumlazimisha mtoto kufanya kazi za nyumbani bila kumuelekeza na kwa kiasi haumfundishi katika uwiano mzuri.

• Kuwapa watoto elimu bora, katika mfumo rasmi na usio rasmi.
• Kuwalea watoto kiroho (misingi ya dini), kimwili, kiutamaduni n.k
• Kuwafundisha watoto katika fani mbalimbali zinazozingatia maadili hasa katika fani unayoona anaipenda zaidi.

Siku zote wazazi wanapaswa kushirikiana, kuheshimiana, kuwajibika na kupendana ili kuweza kujenga familia iliyo bora. Zingatia hayo na hakika utafurahia. Maisha Ndivyo Yalivyo.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment