Monday 26 January 2015

Hadithi-MWANASHERIA KATILI SEHEMU YA 11



Baada ya mwezi mmoja Mr.Cheo aliruhusiwa kutoka hospitalini.Alichukuliwa na polisi kurudishwa gerezani.Kila mara aliingizwa chumba cha mahojiano ili kutoa taarifa zaidi kuhusu tukio la kuuawa kwa watu sita ndani ya chumba alichokuwa amelazwa ila kujibu ilikuwa shida.Alishindwa kabisa kuongea hivyo ilimlazimu kujibu kwa kuandika maelezo kwenye karatasi.Hivyo ndivyo aliwasiliana hata na wafungwa wenzake.
Siku moja wafungwa walihamishwa toka gereza la Tanga mjini mpaka gereza la Segerea.Big Chazi alikuwa ni mmoja wa wafungwa waliohamishiwa gereza la Segerea jijini Dar-es-salaam.Big Chazi ni mfungwa aliyehukumiwa miaka mitano iliyopita kwa kosa la mauaji ya familia yake mwenyewe.Alipewa jina la Big Chazi kutokana na kuwa na mwili mkubwa mno.Jina lake kamili ni Charles Ngumi na alihukumiwa kifungo cha maisha jela

Kutokana na mwili wake huo watu walifikiri alikuwa mtu mbabe na mkorofi sana kumbe alikuwa tofauti.Big Chazi alikuwa mtu mkarimu mno,tena mpenda watu.Alipenda kuwafundisha wafungwa wenzake kuhusu Mungu kwa kipindi chote alichokuwepo gereza la Tanga.Alitoa semina mbalimbali kuhusu maisha na kuwatia moyo wenzake.
Big Chazi alipendwa sana na wafungwa wenzake pamoja na maafisa wa polisi.Siku ilipotangazwa kuwa kuna uhamisho wa wafungwa,jina lake lilipotajwa kuwa miongoni mwa watakaohamishwa,wafungwa wenzake waliobaki walisikitika sana.Hawakutaka Big Chazi aondoke kwani walishamzoea mno.Karandinga liliwashwa,Big Chazi pamoja na wafungwa wenzake wakapelekwa Segerea.
Baada ya Big Chazi kufika Segerea alipelekwa kwenye chumba ambcho pia Mr.Cheo ndiko anakolala.Siku mbili zilipita na Big Chazi alikuwa anamuona mfungwa mmoja akiwa kimya muda wote.Ndipo siku moja akaamua kumfuata amsalimie. “Helloo!samahani bro!mambo vipi?”Big Chazi alishangaa kumwona yule mfungwa akijibu kwa ishara ya kuinua kichwa.
“Unaitwa nani?”Mr.Cheo alikaa kimya tu.Alipanua mdomo na kumwonesha BigChazi.
“Ooooh!!Mungu wangu!!pole sana huna ulimi!!?nini kilitokea?”Mr.Cheo alianza kububujikwa na machozi na kulia kwa kwikwi.
“Pole sana Mungu utakusaidia wala usihofu.Mimi naitwa Big Chazi tutaongea siku nyingine”Big Chazi alimfariji Mr.Cheo na kuondoka.Wiki tatu zilipita na urafiki kati ya Mr.Cheo na Big Chazi uliota mizizi na kutoa matunda bora japokuwa hakuweza kuelewana kirahisi.Siku moja Big Chazi alimwambia Mr.Cheo amweleze kilichomsibu hadi akawa pale gerezani.
Mr.Cheo alichukua kalamu na karatasi na kuanza kuandika kisa chake kuanzia mwanzo mpaka mwisho.Big Chazi aliichukuwa ile karatasi na kwenda kujiegesha kwenye virago vyake vya kulalia ili aisome vizuri.Alijitengeneza kidogo kisha akaanza kusoma taratibu.Kila aliposonga mbele ya story machozi yalimtoka na mara kwa mara alishtuka na kuhisi kitu
“Mbona huyu mchungaji anaemzungumzia mimi nahisi ni Pasta Ndundu!!”alisikitika zaidi aliposoma namna Mr.Cheo alivyokatwa ulimi.Baada ya kumaliza kusoma ile story alifunga macho na kufanya maombi.
Aliomba nusu saa nzima kisha akalala.Kesho yake asubuhi Big Chazi alidamka saa 11 na nusu na kumshukuru Mungu.Baada ya hapo alikwenda kumwamsha Mr.Cheo.
Alipoamka alimwomba afanye naye maombi ya kumshukuru Mungu kwa kuwaamsha salama.Chakushangaza zaidi Mr.Cheo alikataa kabisa kufanya maombi.Big Chazi alihamaki na kujiuliza maswali mwenyewe “Kwanini huyu hataki kumwomba Mungu?”mara kengele ikagongwa na wafungwa wote walitoka kwenda kusikiliza walichoitiwa.
“Mnatakiwa kwenda kupalilia mahindi upande wa Pwani”waljiandaa na kuanza safari ya kwenda shamba.Wakiwa shambani walipalilia kwa bidii mno hasa Mr.Cheo na Big Chazi.Jioni walirudishwa gerezani kuendelea na shughuli nyingine za kawaida.Usiku Big Chazi alimpa pole Mr. Cheo kwa matatizo yote yaliyompata.
“Sasa Mr.Cheo huyo mchungaji mbona kama namjua?”Mr.Cheo alishtuka kidogo.Alichukua kalamu na karatasi na kuandika…
“Unanishangaza sana,unasema unamjua kivipi wakati mimi sijakutajia jina?”Big Chazi alisoma na kutabasamu kidogo.
“Yaani nilivyosoma story yako nimegundua kuwa ni Pasta Ndundu au sio?”Mr.Cheo alishangaa sana na kuandika tena..
“Kwanini umemfahamu mapema hivyo au na wewe ni mmoja wa vijana wake umekuja kunimalizia huku huku gerezani?”
Big Chazi alimwambia Mr.Cheo.
“Tulia wala usiwe na wasiwasi,huyu mchungaji ndio kasababisha mpaka mimi nipo hapa” Mr.Cheo alishtuka kidogo.Big chazi alitulia kimya kwa muda,mara machozi yakaanza kumtoka.Alifuta kisha akamwambia Mr.Cheo “Ngoja nikusimulie kisa chenyewe.
“Mimi nilikuwa mfanyakazi katika shirika la reli hapa Dar-es-salaam.Nilifanya kazi na Pasta Ndundu kipindi hicho kabla hajawa mchungaji.
Miaka miwili ilipita ndipo Pasta Ndundu alipoamua kuacha kazi kwenye shirika hilo na kujikita zaidi kwenye masuala ya uchungaji.Nilishangaa sana kumwona Pasta Ndundu kapata mafanikio makubwa mno kwa kipindi kifupi kiasi hicho.Nilishawishika kumuuliza ni njia gani ametumia hadi akafanikiwa,kwani alitembelea magari ya kifahari,alijenga nyumba nyingi nzuri,pia alikuwa na hoteli kubwa ya kitalii jijini Arusha.
“Tulia nikwambie bwana mdogo”Pasta Ndundu aliniambia nitulie ili anipe siri ya mafanikio yake.Nilitulia na kumsikiliza kwa makini.
“Naomba unielewe na hii iwe siri yako.Mimi nimepata mafanikio haya si kwaajili ya kanisa la hasha!!mimi natumia nguvu za ziada kupata fedha.”Nilishtuka kidogo mara baada ya kusikia nguvu za ziada ndizo zilizomwezesha kupata mafanikio.Nilimkodolea macho na kutega masikio kwa makini sana. “Wewe si u aniona kila wakati nasafiri kwenda nchini Nigeria?”nilimjibu
“Ndio,kwani ukisafiri kuna ubaya?”
“Sasa huko ndipo napoenda kupata usaidizi”niliendelea kumshangaa sana mchungaji yule.
“Pasta Ndundu hebu nenda moja kwa moja kwenye pointi ili nielewe,maana unanichanganya na shortcut zako”Alicheka kidogo kisha akapiga pafu moja ya juice iliyokuwepo mezani.
“Nimejiunga kwenye chama cha Freemasoni!”Nilishtuka baada ya kusikia hivyo kwani nilishawahi kusikia watu waliopo kwenye chama hicho hutumia nguvu za kishetani na ndio maana huwa ni matajiri mno.
“Wala usishtuke ni rahisi sana,ila mimi nataka kukuajiri na nitakulipa ghali sana achana na hizo shughuli za reli hazina faida yoyote.Nataka uwe mmoja wa vijana wangu mtakaokuwa mnasafarisha madawa ya kulevya toka Nigeria mpaka hapa,au unasemaje?”
“Pia unauza madawa ya kulevya?”Kutokana na mshangao nilijikuta nimeropoka kwa kuuliza swali hilo.
“Tulia wewe nikupe dili za pesa”Pasta Ndundu alinishawishi sana na kuniahidi kunilipa kiasi cha sh.milioni 50 kila mzigo utakapofika Dar-es-salaam.Zilikuwa ni fedha nyingi sana kwangu hivyo kutokana na tamaa nilikubali kufanya kazi pamoja naye.Alinionya kwa kuniambia kuwa mpango huu ni siri la sivyo nikimgeuka atanipoteza mara moja.Nilianza kazi lakini kwa kipindi kile ilikuwa ngumu sana kwasababu bado nilikuwa mgeni wa kazi.
Pasta Ndundu alisifika kwenye viwanja vya ndege kwa kugawa fedha kama pipi kwa maaskari pamoja na maafisa ukaguzi.Pindi tulipokamatwa Pasta Ndundu alikuja mara moja na kututoa gerezani.Miezi sita ilipita taratibu nikaanza kuwa mzoefu wa kazi.Nilisafirisha madawa toka nchini Nigeria kupitia Nairobi au Kampala mpaka Dar-es-salaam.Ikifika hapa kuna vijana wengine wa kuisambaza kwa matajiri wanaotumia nchi nzima.
Kutokana na kazi hiyo nilitajirika kwa muda mfupi sana hadi mke wangu akahoji “Hivi mume wangu ni biashara gani hiyo inayokupa mafanikio kiasi hiki?”Kwa kipindi chote hicho sikuwahi kumwambia mke wangu ni kazi gani nafanya baada ya kuachana na shirika la reli.Mama watoto wangu alishangaa sana kwa kuwa kila wakati nilimuaga na kusafiri kwenda nchini Nigeria bila kumwambia naenda kufanya nini?
Alinidadisi kwa muda mrefu lakini hakufanikiwa kupata jibu kwasababu tulifanya kazi hiyo kwa siri kubwa.Hata kipindi nipokamatwa na kuwekwa ndani hakujua kwani nilikaa kwa muda mfupi sana na kutoka.Pasta Ndundu alitumia pesa kama fimbo ya kutulinda.Kwa muda wa miaka miwili tu tayari nilishakuwa bilionea.Nilifungua kampuni ya kusindika maziwa na kiwanda chake,pia nilikuwa na maduka makubwa Kariakoo na magari mengi ya kifahari.
Kutokana na kuwa na utajiri mkubwa kiasi hicho sikuona umuhimu wa kuendelea kuwa punda wa kubeba madawa ya kulevya.Nilimfuata Pasta Ndundu na kumweleza kuwa nimechoka na sihitaji tena kazi yake.Alifoka kwa hasira baada ya kusikia hivyo na kunitishia kuwa atanimaliza.Niliogopa kidogo kwa kuwa nilishashuhudia watu wakiuawa kama kuku na walinzi wa Pasta Ndundu pindi tu walipomsaliti.Nilipiga moyo konde na msimamo wangu ukawa pale pale
“Utakuja kujuta maisha yako yote labla mimi siyo Pasta Ndundu!”Aliendelea kuporomosha maneno makali ila mimi skujali niliamua kuondoka na kuachana naye.Baada ya miezi miwili toka niachane na Pasta Ndundu ndipo kizaazaa kilipoanza kunikuta.Siku moja kiwanda changu kiliungua chote na baadhi ya wafanyakazi waliokuwemo ndani ya kiwanda hicho walikufa wote.Hatuweza kujua chanzo halisi cha tukio hilo ila tulihisi ni itilafu ya umeme.
Ilikuwa ni hasara kubwa sana kuwahi kutokea katika maisha yangu.Mwezi mmoja baadae nilipata janga lingine.Hili lilinifanya mpaka nikachanganyikiwa na kulazwa Muhimbili kwa wiki tatu.Maduka yangu niliyoyategemea yaliyokuwepo Kariakoo yalichomwa moto yote kwa wakati mmoja na watu wasiojulikana.Baada ya kutoka hospitalini nikaanza kuhisi mambo yote haya yanafanywa na Pasta Ndundu.Nilitaka kumfuata nimuulize lakini nikasita.Nilijua ningeweza kuuawa muda wowote.
Kutokana na matukio hayo mawili nikaanza kufilisika.Ili niweze kujikimu mimi na familia yangu ilinilazimu kuuza magari yangu mawili ya kifahari na kubakia na gari moja tu.Mwaka ulipita nikaanza kuhisi umasikini unakaribia kuingia kwenye himaya yangu wakati nilishausahau miaka kadhaa iliyopita.Siku moja nilitoka kwenye mihangaiko yangu mjini nikiwa nimechoka sana.
Nilipofika tu nyumbani nilichokikuta sikuamini.
*************************
Je nini kilitokea baada ya Big Chazi kufika nyumbani kwake?
MTUNZI-FREDY MZIRAY
mliokosa sehemu 10 tumbukia hapa:
http://j2wisdom.blogspot.co.uk/2015/01/hadithi-mwanasheria-katili-sehemu-ya-10.html

No comments:

Post a Comment