Sunday, 11 January 2015

Mume alazimishwa kuacha kazi alee mtoto, mke kazini ! Katika sehemu ya simulizi, kaka huyu anasema; Mzozo wa safari hii umekuwa mkubwa mke wangu akaamua kuondoka kwangu na mtoto wa miaka minne.

Hivi sasa niko mahakamani baada ya usuluhishi Ustawi wa jamii kushindikana. Misukosuko anayonipatia nimeshindwa kuivumilia, hivyo bora tuachane kila mtu afanye mambo yake”, anasema kaka huyu.

Anasema kuwa;”Nilichogundua ni kwamba pale unapompenda sana mwanamke, baadaye hukuona kama fala/bwege fulani na kuanza kukuchezea kama mpira…. Kwangu nimebaini hilo na sasa nasema basi.

“Nachotafuta ni amani yangu, japokuwa amemficha mwanangu naamini iko siku nitamuona tu hata afanyeje. Bora ndoa ivunjike kila mtu afanye mambo yake”, anasisitiza kaka huyu.

Mpenzi msomaji, baada ya kuchapishwa kituko hicho kwenye safu hii, baadhi ya wasomaji wenye mikasa inayotokana na vitimbwi vya wake zao wamefunguka na kutoa yaliyo moyoni.

Ukiona mtu mzima analia, ujue mambo yamemfika shingoni na kuamua kuyatoa hadharani. Au siyo msomaji wangu? Hebu wasikie hawa wafuatao;
…dada Flora, shikamoo. Heri ya mwaka mpya.

Naitwa Meshack naishi Arusha. Ni kijana yatima kwetu nilizaliwa mwenyewe wazazi waliniacha nikiwa na wiki moja nikalelewa na babu mzaa mama.

Nilipokuwa na miaka kumi niliteswa sana na ile familia ya babu na bibi nilianza kuishi maisha ya mitaani huku najisomesha kwa vibarua vya hapa na pale. Nikitoka shule nikawa nalala porini kukikucha naenda chemchem nanawa kisha naenda shule mpaka nikamaliza darasa la saba nikafaulu ila sikupata mtu wa kuniendeleza.

Nikaondoka kijijini kwenda mjini nikafanya kazi nikapanga chumba nikaanza maisha nikabahatika kukutana na binti niliyempenda sana amenipita miaka mitatu, mimi miaka 26, yeye miaka 29.

Bahati nzuri Mungu akatujalia kupata mtoto wa kuime kipindi hicho naishi kwake. Alijifungua kwa operesheni. Kazini nikawa siendi nakaa namwangalia mtoto. Akilia usiku nikimwambia amnyonyeshe anakataa eti atachelewa kuamka kwenda kazini. Asubuhi atamnyonyesha kidogo tu anamweka kitandani.

Tarehe 7.5, 2014 akanitupia mtoto name nikaripoti polisi dawati la watoto. Nikatafuta mama mtu mzima  na hausigeli nikawalipa wakanilelea mwanangu. Mtoto alikuwa na miezi aliponitupia.

Baada ya muda mke na mama yake mzazi wakaniomba tena niwarudishie mtoto nikakataa wakaenda polisi ofisi kubwa mjini wakahonga wakanisingizia kesi ya mauaji nikapelekwa gerezani nao wakamchukua mtoto wangu.

Nilikaa gerezani kwa muda kanisa likaja kunitoa huko na niliporudi nikakuta wamemchukua mtoto wangu, nikaenda polisi kudai nikapewa barua kwenda kudai ustawi wa jamii mtoto wangu.

Wakanijibu nitoe matumizi 80,000 kwa mwezi na sina ruhusa kumuona mtoto wangu. Sina hata ndugu wa kunisaidia, nifanyeje dada Flora?

Mwanamke huyu hadi kupata ujauzito ilikuwa kazi ngumu sana. Nilifungu nikamuomba Mungunae akajibu. Alipopata mimba akajifungulia hospitali ya KCMC.

Nikapambana nikamtunza uzazi, ijapokuwa kiuchumi sikuwa vizuri, lakini baada ya miezi mitatu akabadilika akaanza manyanyaso, akinitesa kwa maneno na mwisho akaniambia chukua mwanao.

Nikaenda kwa mama mkwe kumweleza akasuluhisha ikashindikana na mwisho mama mkwe akaleta hausigeli mwanafunzi wa darasa la nne wamemwachisha shule aje akae na mwanangu nikakataa wakamweka miezi mitatu kwangu, nikamrudisha kwao akaendelee na masomo.

Mke wangu na mamake wakachukia sana kuona nimemrudisha na kuleta binti mwingine wa kazi aliyemaliza darasa la saba. Walichukia mama mkwe wakashauriana na mwane, mwisho mwanamke akamfukuza binti Yule niliomleta mimi.

Matokeo yake nikaacha kazi nikakaa nyumbani kumwangalia mwanangu hadi mke atakapoleta binti mwingine anayetaka na  yeye(mke) akaendelea na kazi na mimi ndio nakaa na mtoto. Hivi ndivyo anavyomalizia ujumbe wake mrefu msomaji wetu.

….Mwingine anasema hivi; “ Ndoa yangu siyo chaguo sahihi maana mke wangu amefikia hatua ya kuleta mabwana ndani kwangu, ila kwa sasa nimetengana naye. Sasa ni zamu yake kunitafuta kwa waganga”, anamalizia ujumbe wake huu mfupi.(mada hii nichaichambua zaidi siku zijazo).

Msomaji wangu, bila shaka umewasikia wenzetu hawa na hasa huyo wa kwanza aliyeeleza historia ya maisha yake hadi hapo alipo lakini bado anaona mlima mrefu mbele yake. Je, unayo yapi ya kumshauri ili atoke hapo alipo?

Anasema yuko peke yake, hana ndugu na matarajio yake makubwa ilikuwa ni kuwa na familia iliyotulia. Tayari Mungu amemfungulia mlango wa uzao, lakini mke aliyedhani angemfaa ndiyo huyo kamgeuka, kamgeuza  hausigeli.

Kazi anaitaka, na mtoto anamtaka, mke alimpenda sana lakini amegeuka na kuwa mcharuko, je, afanyeje sasa? Hebu mshauri.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment