Wednesday, 12 June 2013
FAMILIA YAMKATAA MTOTO WA NGWEA
IKU chache baada ya aliyekuwa mkali wa Hip Hop Bongo, Albert Kenneth Mangweha ‘Ngwea’ kupumzishwa kaburini kufuatia kifo cha usingizini nchini Afrika Kusini kilichotokea Mei 28, mwaka huu, mambo kibao yanazidi kuibuka.
Habari zinadai kuwa familia ya marehemu Ngwea imemkataa mtoto aliyeletwa na mama yake makaburini akidaiwa kuwa ni mtoto wa Ngwea.
MTOTO WA NGWEA
Juni 6, mwaka huu wakati wa mazishi, mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Paulina Jeremiah, mkazi wa Kigamboni, Dodoma alitimba akiwa na mtoto huyo wa kike aitwaye Neema Albert na kudai kuwa alimzaa na Ngwea mwaka 2001, wakati msanii huyo akisoma Sekondari ya Mazengo.
Wakati akijieleza, ndugu wa Ngwea, Anthony Mangweha alikuwa akimsikiliza ambapo aliwataja wanandugu wa marehemu waliokuwa wakijua suala hilo.
Waliotajwa kujua kuwa mtoto huyo alikuwa wa Ngwea ni Frank, Jotam na Amani ambao waliwahi kutumwa na marehemu kwenda kumwangalia mkoani Dodoma.
Hata hivyo, ndugu huyo aliyekuwa akimsikiliza alimtaka mama Neema kupoa, hadi familia ikae kikao.
FAMILIA YAKAA KWA SAA 7, YATOA UAMUZI MZITO!
“Kweli wikiendi iliyopita familia ilikaa kikao kwa zaidi ya saa 7, pamoja na mambo mengine lakini wanadaiwa kufikia uamuzi mzito wa kumkataa mtoto huyo hadi mama Neema apeleke vigezo vya uthibitisho,” kilisema chanzo chetu ndani ya kikao hicho.
Akizungumzia suala hilo kwa sharti la kutotajwa gazetini, mmoja wa dada zake Ngwea alisema: “Ni kweli yule mtoto aliondoka na mama yake lakini kama akileta uthibitisho tutampokea.”
MICHANGO YA RAMBIRAMBI YAHOJIWA
Habari ziliendelea kudai kuwa katika kikao hicho, suala la michango ya rambirambi lilihojiwa huku wanafamilia wakitaka kujua kilichopatikana, kilichopo na namna zilivyotumika.
“Unajua kuna wajanja wengi ‘so’ familia ilikuwa na wasiwasi kuwa inawezekana kukawa na uchakachuaji,” kilidai chanzo chetu.
Ilisemekana kuwa mmoja wa baba wadogo wa marehemu Ngwea alitoa ufafanuzi kwa kumwaga data na kueleza namna zilivyotumika na kiasi kilichobaki ambacho kiliwekwa benki.
MALI ZA NGWEA ZAZUA UTATA
Ilidaiwa kuwa mengine yaliyojiri katika kikao hicho na kuzua utata ni pamoja na mali alizoacha marehemu Ngwea na namna ya kuzikusanya na kuzisimamia.
“Ilisemekana aliwahi kumiliki magari mawili kwa nyakati tofauti lakini aliyauza. Vitu vyake alivyoviacha kwenye nyumba aliyokuwa akiishi Sinza-Mori, Dar vilitakiwa vijulikane ili visafirishwe hadi hapa kwa mama yake,” kilisema chanzo.
Kuna madai kuwa kuna mtu ambaye Ngwea aliwahi kumwambia kuwa alikuwa na kiwanja Goba, nje kidogo ya Jiji la Dar lakini hakuna anayekijua.
Ngwea alifariki dunia Mei 28, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 30 katika kifo tata huko Sauzi.
M 2 THE P HAKUMBUKI KILICHOTOKEA
Wakati huohuo, msanii aliyepata masaibu na Ngwea huko Sauzi lakini akapona, Mgaza Pembe ‘M2 THE P’, wakati anatimua mjini hapa baada ya mazishi, alipotakiwa kueleza kilichowapata hadi Ngwea akafariki dunia, alimwambia mwanahabari wetu kuwa hakumbuki chochote kilichotokea.
Jamaa huyo alidai kuwa bado anaumwa hadi sasa licha ya kuruhusiwa kutoka katika Hospitali ya St. Hellen Joseph ya Afrika Kusini alikolazwa.
chano:globalpublishers.info
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment